This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Wednesday, February 27, 2008

Zanzibar giza siku nne

SHUGHULI za kiuchumi mjini Zanzibar zimesimama kutokana na uhaba wa umeme ulioukumba mji huu kwa siku nne mfululizo sasa.

Uhaba wa umeme ulianza Ijumaa usiku kutokana na nyaya zinazosafirisha nishati hiyo zilizotandikwa chini ya ardhi katika eneo la Mchele na Mlandege kuungua moto.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watumishi serikalini wamelazimika kuzikimbia ofisi zao baada ya kushindwa kufanya kazi kutokana na joto kali lililosababishwa na kukosekana kwa nishati ya kuendesha viyoyozi na kompyuta.

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara nao wamelazimika kuzimwaga bidhaa zao, hasa zile zinazooza kama vile samaki, nyama na matunda baada ya kuharibika kutokana na ukosefu wa umeme.

Aidha, katika maeneo ya Mji Mkongwe, watalii kadhaa walionekana wakihaha kutafuta mawasiliano ili kuwasiliana na watu wengine waliopo nje ya nchi.

Pia baadhi ya wafanyabiashara wa intaneti walilazimika kufunga shughuli zao kutokana na majenereta waliyokuwa wanayatumia kuishiwa na mafuta baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu.

Maeneo yaliyoathirika zaidi na tatizo hilo nyumba ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, eneo la Mbweni, Chupwani, Kiembe Samaki na eneo lote la Mji Mkongwe.

Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar, Juma Isihak, alisema mafundi wanaendelea na juhudi za kurekebisha kasoro hiyo na kwamba tatizo limechukua muda mrefu kushughulikiwa kwa sababu awali mafundi walichelewa kufahamu palipotokea hitilafu hiyo.

“Sifikirii kuleta mafuta kutoka nje, bado mafundi wetu wanaendelea na wanaweza kurejesha hali kama kawaida,” alisema.

Hata hivyo, alisema shirika hilo halina mpango wa kulipa fidia kwa wateja walioathirika na tatizo hilo kwa kuwa limetokea kwa bahati mbaya.

“Hakuna sheria inayotulazimisha kumlipa fidia mteja itakapotokea hali kama hii,” alisema.

Uhaba huo wa umeme pia umesababisha uhaba wa maji mjini Zanzibar kutokana na mitambo ya kusukuma maji kushindwa kufanya kazi.

Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid, alisema uhaba huo wa umeme umeathiri pia huduma ya maji kutokana na mashine kuzimwa.

Baadhi ya wananchi wamelalamika juu ya upatikanaji wa maji ambako sasa dumu la lita 20 linauzwa kati ya sh 400 hadi sh 500.

Walisema iwapo tatizo hilo litadumu kwa muda mrefu, kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko kwa kuwa maji yanayotumiwa na wananchi wengi si salama.

Source: Tanzania Daima, 25/2/2008

No comments: