WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amesema kuwa mikakati yake ya sasa ni kuimarisha zaidi miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ili kuweza kutoa huduma ya umeme katika maeneo mengi zaidi nchini.
Akizungumza na ‘Tanzania Daima’ Dar es Salaam, jana, Ngeleja alisema kuwa mindombinu mingi ya shirika hilo ni mibovu na michakavu, hivyo kazi yake ya kwanza ni kufanya jitihada za kuiimarisha ili iweze kutoa huduma bora ya nishati ya umeme na kwa watu wengi zaidi.
Alisema kuwa mikakati ya kuimarisha miundombinu hiyo ipo mingi, lakini sehemu ya dola milioni 698 (zaidi ya sh bilioni 700) zilizotolewa msaada na Marekani kupitia Mpango wa Changamoto za Milenia (MCC), zitasaidia zaidi kuharakisha jitihada za wizara yake katika kupambana na matatizo ya umeme.
Alisema katika fedha hizo zilizotolewa na Marekani, wizara yake itapata fungu litakalosaidia zaidi kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme hadi vijijini ambako kwa miaka mingi kumekosa umeme kutokana uchakavu wa mifumo ya kufikisha umeme.
“Kazi iliyopo sasa ni kuelekeza nguvu zaidi katika kuboresha mifumo ya kufikisha umeme maeneo mengi zaidi hasa ya vijijini ambako serikali imekuwa ikijitahidi, lakini uwezo ndio unaosumbua,” alisema Ngeleja.
Aliongeza kuwa juhudi za kuimarisha mifumo ya umeme itapewa kipaumbele katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam, Morogoro, Mbeya, Tanga na Kigoma.
Alisema kuwa maeneo hayo yamekuwa na shida kubwa ya umeme, na kuongeza kuwa mbali ya mikoa hiyo pia wataangalia maeneo mengine ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa manufaa ya umma.
Kuhusu suala la kupunguza bei ya umeme kwa watumiaji, alisema kwa sasa jukumu ambalo lipo mbele yao ni kuona jinsi watakavyoweza kuboresha kwa upatikanaji wa huduma na baada ya hapo mamlaka husika zikiwamo Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (Ewura) itaweza kutoa mapendekezo ya bei ya ulipaji wa nishati hiyo.
“Jukumu la kuongeza ama kupunguza bei ya umeme litafuata taratibu zake zinazoangalia mambo mengi ya msingi, hivyo ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba kwanza ni kuona wapi tunaweza kufanikiwa zaidi kwa kupeleka huduma ya umeme na mambo mengine yatafuata baadaye,” alisema Ngeleja.
Source: Tanzania Daima
This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.
Saturday, February 23, 2008
Ngeleja ataka umeme usambae nchini kote
Posted by
Godfrey
at
18:58
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment