This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Thursday, November 15, 2007

Mwalimu Andoya aokoa kijiji kwa kubuni mradi wa umeme

KATIKA dunia ya sasa watu wamejaliwa kuwa na vipaji vya aina mbalimbali.

Baadhi ya vipaji hivyo vinaweza kuwaletea maendeleo na vingine vinakosa kuendelezwa, kutokana na kukosekana wafadhili wa kuwasaidia watu wenye vipaji hivyo.

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alikuwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kujionea hali halisi ya umeme katika wilaya.

Katika safari yake hiyo, Ngeleja alibahatika kukutana na Mkurugenzi wa Mradi wa Ujenzi wa Umeme wa Nguvu ya Maji, Menas Andoya. Mkurugenzi huyo amebuni mradi huo na kuutengeneza katika mto Mtandazi wilayani Mbinga.

Hivi sasa mradi huo unawasaidia wanakijiji hao kukoboa na kusaga nafaka mbalimbali.

Andoya anasema yeye ndiye alibuni mradi huo wa ujenzi wa umeme wa nguvu ya maji. Ulifanyiwa utafiti mwaka 1998 – 2001 na kuupatia jina la Nguvu ya Maji Partnership. Mwaka 2003 mradi huo ulisajiliwa na kuitwa Andoya Hydro Electric Power Co.Limited (AHEPO LTD).

Kitaaluma, Andoya alikuwa mwalimu wa shule ya msingi wilayani humo na baadaye aliamua kujifunza ufundi wa magari.

Ni ufundi huo wa magari ndio uliompatia mwanya wa kuchukuliwa na Mjerumani katika shughuli zake kama fundi magari.

Andoya anasema utaalamu huo ameweza kuupata, kwa sababu alikuwa anafanya kazi na wajerumani.

Anasema kuwa wakati mwingine walikuwa wakikaa maporini, ambapo iliwalazimu kutafuta vyanzo vya mito ili kutengeneza nishati ya umeme, ambayo uliweza kuwasaidia wakiwa huko.

Baada ya muda, Wajerumani hao walirudi kwao na yeye kuamua kurudi kijijini kwake Lufakara, kwa ajili ya kujishughulisha na shughuli nyingine za kumletea kipato.

Andoya anasema kutokana na kupata mbinu mbalimbali za uzalishaji wa umeme, aliweza kubuni mbinu ya kuondoa tatizo la umeme kijijini hapo.

Alianza kwa kufanya utafiti katika misitu na kutembelea vijito mbalimbali, vinavyounganisha mto Mtandazi

Andoya anasema baada ya utafiti huo aliweza kuomba msaada kwa Mhandisi, Godfrey Ndevo, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya umemem wa maji.

Ndevo aliweza kumsaidia katika kuhakiki utafiti na kuchukua vipimo vya maporomoko ya maji, kisha kuvipeleka kwa wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuthibitisha au kupata uhakika wa utafiti huo.

Andoya anasema mpaka sasa ameweza kutengeneza nguvu ya umeme ya kilowati 30, kwa kutumia nguvu ya maji.

Alifanikisha malengo ya mradi huo, kutokana na ufadhili wa fedha alioupata kutoka kwa Wajerumani, ambao walimpatia kiasi cha Sh milioni 250.

Katika awamu ya kwanza, mradi huo wa umeme wa maji ulikuwa unaendesha mashine za kusaga nafaka na awamu ya pili ilihusu kuwasha taa za umeme wa moja kwa moja, kutokana na betri zinazochajiwa kwa nguvu ya maji. Awamu ya tatu ya mradi huo inahusu kuzalisha umeme, utakaokuwa na nguvu ya megawati 1.2.

Andoya anasema katika kutekeleza mradi huo, amefanikiwa kuanzisha huduma ya kusaga nafaka kwa bei nafuu kutokana na vinu, hivyo kutumia nishati ya nguvu ya maji na mafuta ya dizeli .

Andoya anasema kutokana na nguvu hiyo ya umeme na vinu hivyo, zaidi ya wananchi 600 kutoka vijiji vya Uzena, Mkwaya , Kilimani na Mbangamao, wameweza kunufaika na huduma hiyo.

Aidha, Andoya anasema mashine ya nguvu ya maji aliweza kuiunda mwenyewe, lakini baada ya muda mashine hiyo ilishindwa kufanya kazi, hivyo ilibidi awasiliane na Wajerumani hao na kuweza kumsaidia kumpa mashine ya kuzalisha nguvu ya umeme, ambayo imeweza kumsaidia hadi sasa katika kusaga nafaka kijijini hapo.

Andoya anasema baada ya kutatua tatizo hilo, aliweza kubuni mradi wa pili, ambao ni kuzalisha umeme wa megawati 1.2 kwa kutumia nguvu ya maji.

Andoya anasema anatarajia kuupeleka umeme huo makao makuu ya wilaya hiyo na vijiji vya jirani, ikiwa ni pamoja na kurudisha uoto wa asili kwa kupanda miti na mimea iliyokuwapo awali, hasa kwenye vyanzo vya mito vinavyopeleka maji kwenye mto Mtandazi na kuzunguuka eneo la mradi.

Andoya anasema anasubiri kupata vibali vya serikali ili waweze kuzalisha umeme wa megawati 1.2 .

Andoya anasema sasa hivi anashughulikia kupata kibali kutoka serikalini. Kibali hicho ni cha TANESCO juu ya ununuzi wa umeme huo, kwani TANESCO ndio wenye kibali cha kumiliki umeme huo, hivyo mgunduzi lazima asubiri mazungumzo kati ya TANESCO na serikali ili mgunduzi kukubaliwa kununua umeme huo.

Andoya anasema katika mradi huo, amekwama kupata kibali cha kuutambua mradi huo kutoka Wizara ya Nishati na Madini kupitia TANESCO, ikiwa ni pamoja na cheti cha uhifadhi wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Andoya anasema mradi huo umeshafanyiwa upembuzi yakinifu, ikiwa ni pamoja na utafiti wa athari za mazingira (I.E.A), pia una hati miliki za ardhi na maji na kwamba mamlaka za utoaji wa vibali, leseni na ushauri zimeshirikishwa.

Aidha Andoya anasema awamu ya tatu imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, ikiwa ni pamoja na utafiti wa athari za mazingira pamoja na hati miliki za ardhi na maji zimekamilika.

Anasema mamlaka za utoaji leseni na ushauri zimearifiwa na kushirikishwa juu ya mradi huo wa umeme .

Andoya anasema mradi huo utakapokamilika utazalisha uniti 8,400,000 za umeme kwa mwaka, ambapo matarajio ya mapato ya mradi huo kwa mwaka ni Sh 648,000,000.

Anasema mradi huo unatarajiwa kuokoa matumizi ya mafuta ya dizeli ya lita 1,900,000 kwa mwaka.

Anasema mradi huo utakapokamilika, serikali itaweza kupata milioni 30 kwa mwaka kama kodi, inayotokana na uzalishaji huo wa nguvu ya maji.

Andoya anasema mpaka sasa ameweza kuwaajiri wafanyakazi watatu, ambao wanamsaidia kutengeneza mashine na kusaga na kukoboa.

Wakati mwingine wateja wanaokwenda kusaga nafaka wakipungua, husaidiana na wafanyakazi hao kupanda miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.

Andoya anasema ingawa anapata fedha kidogo, kutokana na mashine hizo, lakini bado hali yake ni mbaya, kwani maendeleo yoyote yanahitaji fedha.

Lakini kama Tanesco watakubali kununua umeme huo, ataweza kunufaika kwa asilimia kubwa kimaisha.

Anaeleza kuwa mradi huo unatarajia kuibua ajira binafsi na kusaidia shughuli za viwanda vidogo vidogo, hospitali, maofisi, viwanda vya kukoboa kahawa, kuinua elimu na kuongeza taaluma ya teknolojia, hasa shule za msingi na sekondari za eneo la mradi huo.

Andoya anasema ameshapanda miche 65,000 ya miti mbalimbali kwenye eneo la mradi, ikiwemo miti 15,000 ya asili, ambayo imeoteshwa na kurutubishwa kwenye viriba kutokana na vikonyo na mizizi na pembezoni mwa barabara. Pia miti ya maembe ili wananchi waweze kupata matunda hapo baadaye.

Mwanakijiji wa kijiji cha Lufakara, Hassani Mwanikola, alimshukuru Andoya kwa kuweza kuanzisha mradi huo wa umeme kijijini hapo.

Anasema hapo awali walikuwa wakipata taabu ya kusaga mazao yao, kutokana na umbali uliopo kutoka vijiji hivyo hadi mjini.

Mwanikola anasema wanapokwenda kusaga nafaka zao, wanatozwa fedha kidogo. Anasema wameweza kupunguza safari za kwenda mjini, kutokana na kupata huduma hiyo kijijini hapo.

Kwa upande wake, Ngeleja alimpongeza Andoya kwa kubuni mradi huo, ambao umeweza kuwasaidia wananchi kukoboa nafaka zao na pia kuweza kuwapatia umeme baadhi ya wananchi.

Ngeleja anasema serikali ya Awamu ya Nne inasisitiza na kutambua michango ya wajasiriamali hasa wawekezaji wazalendo, ambao wanawekeza katika nchi yao, badala ya kuwa wafanyakazi kwa wawekezaji wageni.

Hivyo, alimtaka Ndoya kuwa mvumilivu wakati maombi yake ya kupatiwa leseni ya kuzalisha umeme yakishughulikiwa.

Source: HabariLeo; Thursday,November 15, 2007 @00:04

1 comment:

upperwater said...

Nimefurahi kwa taarifa ya kufua umeme.ninge penda kujua je nilazima kuwauzzia tanesco huo umeme...sijajua kwa nini wizara ya nishati haija itambua.
pia je ni vibali gani vinahitajika
ili kuweza kuanza kuzalisha umeme kijiji kama wa 1.0Mega wati.
Asante