This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Wednesday, November 21, 2007

Umeme wazidi kuleta kilio

MPANGO wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutaka kupandisha gharama za umeme umezidi kupingwa na wadau mbalimbali, huku wakidai uzembe wa wafanyakazi wa shirika hilo kushindwa kukusanya madeni ndiyo chanzo cha shirika kushindwa kujiendesha kibiashara.

Wadau hao ambao walizungumza jana kwenye mikutano iliyoitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) katika mikoa ya Mwanza na Arusha, walisema shirika hilo sasa linataka kuficha udhaifu, kuwatupia mzigo wananchi na kuwaongezea machungu na makali ya maisha.

Tanesco imependekeza kuongeza bei ya kuunganishiwa umeme na malipo ya ankara kwa asilimia 40 mwakani.

Wadau wanadai iwapo gharama hizo zitapanda, umeme utakuwa ni anasa kwa Watanzania, huku wananchi wa vijijini wataendelea kuishi bila kupatiwa huduma hiyo.

Kati ya Watanzania milioni 38 ni asilimia saba tu ambao wanatumia nishati hiyo huku maeneo mengi ya vijijini hawana huduma hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Umeme, Profesa Jamidu Katima, alisema katika maombi ya Tanesco kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kuiruhusu ipandishe gharama za umeme haikuwasilisha mchanganuo unaotakiwa.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika mjini Mwanza, Profesa Katima alisema Tanesco imeomba kupandisha ankara ya umeme kwa asilimia 40 na gharama za kuunganisha umeme asilimia 196 na 281 bila kuambatanisha mchanganuo mzima.

“Kama hivyo ni kweli baraza halioni ni vipi gharama za kuunganisha wateja zipandishwe, mfano service line ya njia tatu ipande kutoka Sh 280,000 hadi Sh 1,065,735,” alisema Katima na kuongeza kuwa shirika hilo lilipaswa kuwasilisha mchanganuo unaoonyesha gharama halali za kununulia vifaa kuonyesha uhalali wa ongezeko waliloliomba.

Alisema baraza hilo limeona gharama kubwa za uendeshaji ambazo zinaonekana ni za Tanesco, hasa katika maeneo ya kushindwa kukusanya madeni, hujuma kwenye miundombinu, wizi na upotevu wa umeme ambao kwa sasa ni zaidi ya asilimia 24 tofauti na kiwango kinachokubalika cha kimataifa cha asilimia 12.

Tatizo jingine la shirika hilo ni kuingia mikataba ghali ya IPTL na umeme wa Songas na kwa mantiki hiyo si haki kuwabebesha mzigo huo watumiaji. “Tanesco walitakiwa wawasilishe mpango kabambe wa shirika ukionyesha hali halisi, lakini haukuwasilishwa,” alisema.

Profesa Katima alisema kushindwa kwa shirika hilo kutoa mchanganuo wa gharama za kutoa huduma za umeme na kushindwa kuwasilisha mpango kabambe, baraza hilo limeshindwa kujiridhisha na mikakati ambayo Tanesco imejiwekea ya kupunguza gharama zisizo za lazima.

Alisema kwa kuwa shirika hilo linaona yupo mtu wa kulipia gharama hizo, halitoweza kuona umuhimu wa kupunguza hizo gharama na ndiyo maana makadirio yake yanazidi kupanda mwaka hadi mwaka katika mpango wake ambao uko hadi mwaka 2012.

Mwenyekiti huyo alisema ankara zilizopendekezwa na shirika hilo zimeonyesha kuwa baadhi ya makundi ya watumiaji wa umeme yanafidiwa na makundi mengine kwa maana hiyo kuna usiri fulani.

“Kwa kuwa wengi wa watumiaji wa makundi hayo ni wazalishaji wa viwanda, baraza lina hofu kuwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda zitakuwa za bei kubwa na hivyo kuathiri watu wa kawaida,” alisema.

Mjini Arusha Mwenyekiti wa Baraza la Watumiaji Umeme mkoani humo, Mhandisi Mubezi Deogratius Lutaihwa alisema haoni sababu ya Tanesco kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 40, kwani utendaji kazi wa shirika hilo ndiyo kikwazo cha kushindwa kufanya kazi kibiashara na kupata faida.

“Kwanza takwimu nyingi zilizoelezwa hapa zina dosari nyingi na walipaswa kuandaa masterplan (mpango kabambe) ya mpango wa maendeleo yao badala tarakimu hizi ambazo zinazua maswali mengi zaidi,” alisema.

Meneja wa Kiwanda cha mbao cha Fibreboard Ltd, Spous Mushi alisema mpango huo utaleta madhara makubwa kwa uchumi, kwani wamiliki wa viwanda watalazimika kupunguza idadi kubwa ya wafanyakazi wao.

“Hii italeta madhara kwani watakaopunguzwa wanaweza kujiingiza katika vitendo vya uhalifu kama ujambazi na unyang’anyi kutokana na kukosa ajira, lakini wanawake walioajiriwa waliopunguzwa wanaweza kuwa machangudoa,” alisema huku akishangiliwa na watu walihudhuria mkutano huo.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda mkoani hapa (CTI), Anup Modha alitaka shirika hilo liache kuendeshwa kisiasa na kuingia mikataba ya biashara ambayo ina hasara.

Alisema haoni kwa nini mzigo huo ulipwe na wateja wa kawaida kwa kuwapandishia bei ya umeme.

Naye Ibrahim Hasi, ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyerere mjini Mwanza, alisema shirika hilo lingejaribu kuweka utaratibu kama wa Mamlaka za Maji nchini ambao umeweka viwango tofauti kwa kila mdau kwa watumiaji wa nyumbani na viwandani kabla ya kupandisha bei.

Source: Habari Leo, 20/11/2007

No comments: