This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Wednesday, November 07, 2007

TANESCO HAPANA!

Majira

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza gharama mpya za kuwaunganishia umeme wateja wapya.

Katika mabadiliko hayo, gharama za kuunganisha umeme kwa njia moja (single phase) imepanda kutoka sh. 240,000 hadi sh. 563,271.

Mabadiliko hayo ya bei pia ni kwa wanaotaka kuunganishwa umeme wa njia tatu (three phase) ambazo ni kubwa kuliko hizo za single phase.

TANESCO imetoa sababu mbalimbali za kufikia uamuzi huo wa kupandisha gharama hizo za kuunganisha umeme.

Je, kipi kilistahili kuwa cha kwanza kwa TANESCO, kuimarisha huduma zake kwa wateja au kupandisha bei ya huduma inazotoa?

Hilo ndilo swali ambalo bila shaka wananchi wanaotarajia kupata huduma inayotolewa na TANESCO pekee wanajiuliza.

Takwimu zinaonesha ni asilimia kumi tu ya Watanzania ndiyo wanaotumia huduma ya umeme.

Hali hiyo imesababishwa na mambo mbalimbali, moja ikiwa ni kushindwa kumudu gharama za kulipia huduma hiyo ikiwemo ya kuunganishiwa.

Lakini wakati Serikali iko katika kampeni ya kupambana na mazingira ikihamamisha watu waache kutumia kuni na mkaa, TANESCO ndiyo hao wanapandisha gharama za huduma zao.

Kwa hali hiyo ni wazi kuwa kampeni ya kupambana na uhalibifu wa mazingira haitafanikiwa, kwani asilimia ya Watanzania wanaotumia umeme huenda ikashuka badala ya kupanda.

Pamoja ni uamuzi huo wa TANESCO, tunatarajia Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA) itasema lolote katika suala hili.

Kama imepitisha bei hizo itakuwa haijatutendea haki wananchi, na kama haijafanya hivyo iingilie kati mara moja.

Source: Majira

No comments: