This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Monday, October 22, 2007

Waliounganishiwa umeme kinyemela Arusha wajisalimisha

Majira

Waliounganishiwa umeme kinyemela Arusha wajisalimisha

Na Said Njuki, Arusha
WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likijipanga kukabiliana na hujuma dhidi ya upotevu mkubwa wa nishati hiyo, wananchi wengi waliounganishiwa laini za umeme kinyume cha sheria mjini hapa, wamejisalimisha.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza katika ofisi za shirika hilo wakiomba kukaguliwa laini zao na hatimaye kusajiliwa rasmi ikiwa ni katika kuonesha kuwa hawataki matatizo.

Mji wa Arusha ni moja ya miji iliyokubwa yenye laini nyingi za umeme zinazodaiwa kuunganishwe kinyume na sheria na watumishi feki wa shirika hilo maarufu kama Vishoka ambao huwadaka wateja halali na kuwaunganishia umeme kinyemela.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Bw. Boniface Njombe alikiri kuwepo kwa wimbi hilo la wananchi wanaojisalimisha na kuhitaji kuunganishiwa umeme kihalali ili kuepukana na matatizo yanayoweza kuwapata baada ya kubainika.

Bw. Njombe alisema shirika limejipanga vizuri kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya operesheni ya kuwaunganishia wateja wake umeme kwa wakati hali iliyokuwa ikikwamishiwa na uhaba wa vifaa kwa ajili hiyo.

Aliwataka wananchi kuepukana na vishoka ambao wanaweza kuwatia matatani siku zijazo kwa kile alichosema shirika litafanya uhakiki wa uunganishaji wa laini za umeme ili kubaini uhalali wake.

"TANESCO imekuwa ikihujumiwa na vishoka kwa muda mrefu na wakati hujuma hizo zikiendelea, shirika lilikuwa likiendelea kupokea maombi mengine ya kuunganishiwa umeme hali iliyosababisha shirika kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja wake hasa kutokana na uhaba wa vifaa," alisema Bw.Njombe.

Aliongeza kwamba shirika limejipanga na kwamba linakabiliana na hali hiyo na siku za vishoka hao kuishi kwa mgongo mwa TANESCO zinahesabika.

Source: Majira, 22/10/2007

No comments: