This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Saturday, October 20, 2007

‘Elimu ya nishati mbadala yahitajika’

‘Elimu ya nishati mbadala yahitajika’

na Hellen Ngoromera


SERIKALI imeshauriwa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala ya mkaa.

Wito huo ulitolewa jana na Meneja Masoko na Uhusiano wa Kiwanda cha kutengeneza mkaa cha East Africa Briquette Ltd chenye maskani yake mkoani Tanga, Happyfania Ngonyani, wakati wa maonyesho ya hatimiliki ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Ngonyani, alisema ikiwapo jamii itaelimishwa juu ya matumizi sahihi ya nishati hiyo itasaidia kuhifadhi mazingira na kuhifadhi maliasili zilizopo kwa kuwa hakutakuwa na ukataji miti.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kiwanda hicho kilipata ubunifu wa utengenezaji wa nishati hiyo baada ya kujifunza kutoka Afrika Kusini ambao kwa kiasi kikubwa hutumia nishati hiyo.

“Awali tulikuwa na kiwanda cha kukusanya taka zitokanazo na masalia ya shambani kama vifuu vya nazi, pumba na mengine, lakini baada ya kutembea katika nchi za wenzetu tuligundua kuwa wanatumia taka hizo kutengeneza mkaa nasi tukaanzisha kiwanda kwa kazi hiyo,” alisema.

Alisema, kwa sasa soko lao linatokana na upatikanaji wa wateja wengi hasa Afrika Kusini na Oman, huku akibainisha kuwa kwa hapa nchini soko la nishati hiyo ni dogo sana kutokana na wananchi wengi kushindwa kuelewa faida za matumizi ya nishati mbadala.

“Tunapata oda nyingi kutoka kwa nchi za wenzetu kwa siku tunazalisha tani 15 hadi 20 za mkaa…hivi karibuni tulipeleka nje tani 72,” alisema na kuongeza kuwa uzalishaji wa nishati hiyo unawasaidia vijana kupata ajira kwa kuuza malighafi mbalimbali kama vifuu vya nazi na mapipa kiwandani kwao na kujipatia fedha.

No comments: