This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Saturday, April 05, 2008

Muswada wa umeme wapigwa danadana

HATIMA ya kupelekwa bungeni kwa muswada wa sheria mpya ya umeme, imezidi kuchukua sura mpya baada ya Kamati ya Nishati na Madini kushindwa kutoa msimamo wake na kuahidi kuutoa Ijumaa ijayo mjini Dodoma wakati wa vikao vya Bunge.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Nswanzugwanko, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umamuzi wa kamati hiyo.

Alisema muswada huo ulikuwa moto zaidi kutokana na baadhi ya wabunge kutokubaliana nao kutokana na kuonekana una lengo la kuliua Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kuzipendelea zaidi kampuni zitakazokuja kuwekeza katika sekta ya umeme.

Alisema Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliwasilisha baadhi ya mabadiliko yaliyoshauriwa na baadhi ya wabunge katika semina ya kujadili muswada huo wiki iliyopita, ambapo kwa kiasi kikubwa amejibu na kurekebisha matatizo yaliyoonekana.

Alisema kamati imemuamuru Waziri Ngeleja kwenda kuyaandika vizuri zaidi majibu yake na ayawasilishe katika kikao kijacho ambacho kitafanyika mjini Dodoma.

“Haya masuala ni nyeti sana na tunahitaji kujipanga vizuri ili tuweze kwenda mbele zaidi na pia kuepukana na masuala yaliyotokea katika mkataba wa Richmond,” alisema Nsanzugwanko.

Aidha, alikanusha tuhuma zilizoenezwa na baadhi ya watu kuwa kamati yake imerubuniwa na serikali, ili ipitishe muswada huo ambao ulizua utata mkubwa miongoni mwa wabunge wiki iliyopita.

Alisema kamwe kamati yake haiwezi kurubuniwa kwani kila mbunge ana kiu ya kuwa na umeme katika jimbo lake, ili uweze kuharakisha maendeleo na kutokomeza umasikini miongoni mwa jamii.

Awali, baada ya kutokubalika kwa muswada huo na wabunge katika semina iliyoandaliwa, Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, walilazimika kutumia nguvu nyingi kuwashawishi wabunge ambao walionekana kutoelewa somo.

Source: Tanzania Daima, 05/4/2008

No comments: