This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Saturday, April 05, 2008

Moto kuwaka bungeni keshokutwa hoja ya Richmond kuibuka upya

WIKI ijayo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kupata mtihani wake wa kwanza bungeni atakaposimamia mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya watu waliohusika katika kashfa ya Richmond.

Mtihani kwa Pinda unakuja kutokana na kuwapo taarifa kwamba suala hili la Richmond limewagawa wabunge katika sehemu mbili.

Wapo baadhi ya wabunge ambao wanadaiwa kuwa kambi moja na baadhi ya watu wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo wakiendesha kampeni ya kuhakikisha suala hilo linakosa nguvu ya kujadiliwa katika kikao hicho na wengine wanaokwenda na mtazamo wa Watanzania.

Wabunge hawa pamoja na baadhi ya wana CCM wenye ushawishi mkubwa ndio ambao pia waliweka kambi Butiama wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kuhakikisha kuwa hoja ya mafisadi kuchukuliwa hatua kichama inaizimwa.

Hata hivyo, wapo wabunge ambao wanapa na kuhakikisha kuwa suala la Richmond linajadiliwa na watu wote waliohusika na kashfa wanachukuliwa hatua bila upendeleo.

Joto la kashfa ya Richmond limezidi kuongezeka baada ya wiki hii bunge kutoa taarifa iliyokuwa ikituhumu kuwapo kwa kundi la watu nchini linaloeneza uvumi wa kutaka kumchafua Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano, Samuel Sitta.

Taarifa hiyo ya bunge ilikwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba njama hizo za kutaka kumchafua spika kumhusisha na ubadhirifu wa fedha za bunge zimekuja hivi sasa wakati bunge bado linashunglikia suala la Richmond.

Ni kutokana na hali hiyo ya mvutano mkubwa kuhusu Richmond, Waziri Mkuu Pinda atakuwa na mtihani kama kiongozi wa serikali bungeni kusimama kidete kuhakikisha kuwa ahadi yake ya kuona watu waliohusika na kashfa ya Richmond wanachukuliwa hatua zinazoshaili inafanyika.

Kama atakwama kusimamia serikali kuwachukulia hatua au timu aliyoiunda ambayo kwa mara ya kwanza ilimaliza kazi mapema kabla ya muda wake itakuja na mapendekezo hafifu ambayo haya maslahi kwa nchi, huenda ndiyo ikawa safari ya Pinda kuanza kuporomoka.

Wananchi bado wana imani na Pinda wanajua kwamba ni waziri mkuu mwenye msimamo ambaye husema kweli bila kuuma umma maneno yake.

Katika bunge lililopita aliapa kuwa wale wote watakaobainika kuhusika na kashfa hiyo bila ya kujali nyadhifa zao serikalini au ndani ya chama, watachukuliwa hatua za kisheria kama kawaida.

Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaona Pinda ana kibarua kigumu kuwabana watu waliohusika katika kashfa hiy kutokana na ukweli kwamba ni watu wenye 'nguvu' hata ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wana mizizi kiasi kwamba chama kinawagwaya.

Ukweli huu unadhihirishwa na kitendo cha CCM kushindwa kujadili hoja ya kuwachukulia hatua kichama watu wanachama ambao wanadaiwa kuchafuka kutokana na kuhusika katika kashfa za ufisadi.

Hata hivyo, Pinda naye ameanza kujitenga na mtihani huo, kwani hivi karibuni alikaririwa akisema kwamba baada ya kuipokea ripoti hiyo ataifanyia kazi na hatimaye kuiwasilisha kwa Rais Jakaya Kikwete kwa hatua na maelekezo yake.

Ripoti ya tume hiyo inafuatia taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa Zabuni ya Kampuni ya Richmond ya Houston, Texas Marekani ambapo Wabunge hao walijadili taarifa hiyo na kutoa jumla ya mapendekezo 23 ambayo serikali iliahidi kuyafanyia kazi.

Timu hiyo ya Pinda inahusisha wawakilishi kutoka Ikulu, sekretarieti ya mawaziri,Tume ya maadili, TAMISEMI, Wakala wa Manunuzi (PPRA), Makandarasi, Utumishi wa Umma na Mipango, itapitia mapendekezo hayo na kutoa dira ya namna ya kuyatekeleza.

Tume hiyo iliundwa kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Bunge Iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali kwa waliohusika na kashfa ya Richmond.

Alitaja baadhi ya mapendekezo hayo kuwa Msajili wa Ofisi ya BRELA kuifuta Kampuni ya Richmond na wamiliki wake wote kufunguliwa kesi ya jinai, kisha serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha malipo kwa kampuni ya Dowans.

Alisema serikali pia ilitakiwa kuendesha uchunguzi wa kina kubaini taarifa tete kuwa taarifa ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuhusu Richmond ilichezewa na kuitafuta taarifa halisi ya taasisi hiyo.

Mapendekezo mengine ni serikali kujiepusha na utaratibu wa matumizi ya mawakala katika manunuzi ya Umma, Sheria ya manunuzi (PPRA) ipewe meno zaidi na ifanye kazi kwa kujitegemea bila kusimamiwa na Wizara ya Fedha.

Kamati hiyo pia ilipendekeza serikali kupitia upya mikataba yote na kuweka kumbukumbu ya mikataba hiyo katika ofisi za bunge, timu ya Serikali inayoshauri mikataba (GNT) iwajibishwe, aliyekuwa waziri wa nishati na Madini, Nazir Karamagi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wawajibishwe.

Wakati huo huo, wabunge sita wanatarajia kutoa hoja binafsi zitakazojadiliwa katika kikao cha bunge hilo.

Siku za hivi karibuni Wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wameonekana kuwa mwiba kwa serikali ambapo wamekuwa wakihoji bila woga utendaji wake kwa maslahi ya wananchi.

Wabunge hao kila mmoja tayari wamepeleka hoja binafsi katika maeneo tofauti huku wengi wao wakihoji moja kwa moja utendaji wa serikali na matumizi mabaya za umma.

Wabunge waliopeleka hoja binafsi ni Raphael Chegeni (Busega), William Shellukindo (Bumbuli), Alloyce Kimaro (Vunjo), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), wote wa CCM na mmoja kutoka Chadema, Said Arfi (Chadema).

Source: Mwananchi, 5/4/2008

No comments: