*Wataka viongozi waliosaini mkataba washitakiwe haraka
*Wadai wanachangia kuiua kwa mikataba mibovu, gharama
WAFANYAKAZI wa Shirika la Umeme (Tanesco) wamecharuka na kutaka viongozi na watendaji wengine serikalini walioliingiza shirika hilo katika hasara kwa kusaini mkataba na kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, washitakiwe haraka.
Katika mkutano wao uliofanyika mapema leo makao makuu, wafanyakazi hao walisema baadhi ya viongozi ndani ya serikali wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanesco inakufa, ndiyo maana wanaliingiza kwenye mikataba waliyoiita ya kinyonyaji.
“Yaani Tanesco imegeuzwa mwarobaini, kila mtu analeta mkataba wake ili anyonye na kuondoka,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Tanesco, Abdul Mukama.
Alisema mkataba wa Richmond ambao ulipigiwa kelele na wafanyakazi wa shirika hilo, unadhihirisha namna viongozi wa siasa walivyodhamiria kuhakikisha shirika hilo linakufa kutokana na fedha zinazolipwa na shirika hilo kwenda kwenye kampuni binafsi.
Mukama alisema wafanyakazi kwa muda mrefu wamekuwa wanajituma kuhakikisha shirika hilo linainuka, lakini tangu serikali iingie mkataba na kampuni ya IPTL, Songas, Aggreko na sasa Richmond, zimekuwa zinalipwa fedha nyingi na shirika hilo.
“Mimi sioni kama hawa walistahili kujiuzulu, hawa wanatakiwa kukamatwa na kushitakiwa haraka,” alisema Mukama wakati akifungua mkutano huo ambao ulikuwa unajadili suala hilo la mkataba wa Richmond.
Mukama alisema mtu wa kwanza ambaye alitaka kuiua Tanesco ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye aliingiza menejimenti ya Afrika Kusini kwa nguvu ambayo pia haikuleta ufanisi wowote zaidi ya kuuza mali za shirika hilo na kuliacha likiwa hoi kifedha.
Alisema Rais Mkapa aliipeleka Tanesco kwa dalali ambaye ni Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa miaka 10. Alisema katika kipindi hicho shirika hilo halikuruhusiwa kuingia katika mkataba wa aina yoyote ile mkubwa, hali iliyosababisha miundombinu yake kuchakaa.
Baadhi ya wafanyakazi wengine ambao walipata fursa ya kuchangia kwenye mkutano huo, walisema viongozi wa siasa wakiwamo wale ambao wameingia mkataba wa Richmond, wameshiriki kuidhoofisha Tanesco.
“Rais Kikwete ameelemewa na ufisadi wa watangulizi wake. Haya yanayofanyika ndani ya Tanesco yameanza siku nyingi, anashindwa afanye nini kama anataka kusafisha uozo, ni vyema pia amshitaki Rais mstaafu,” alisema Thomas Njumayo.
Walisema kitendo cha kampuni ya Richmond na sasa Dowans kulipwa Sh bilioni 4.7 kwa mwezi na Tanesco inaonyesha namna ambavyo viongozi wa siasa wasivyokuwa na uchungu na shirika hilo.
Mfanyakazi mwingine alisema ni vyema serikali iilipe fidia Tanesco kwa vile katika miaka minane shirika hilo limeathirika kwa kiasi kikubwa, ikiwamo kupoteza chuo chake cha Morogoro kilichokuwa kinatoa wataalamu wa hali ya juu.
Alisema pia Tanesco inatakiwa kulipwa faida, kwa vile menejimenti ya Netgroup iliuza baadhi ya majengo katika hali ya kutatanisha, huku wakiliacha shirika likiwa katika hali mbaya ya fedha.
Mfanyakazi mwingine aliyejitaja kwa jina la Mwakugile alitaka wafanyakazi hao waazimie kama fedha hizo zinalipwa kutoka hapo Tanesco wazizuie, ziweze kuongeza ufanisi wa shirika hilo.
Suala la Richmond lilitokana na ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyokuwa inaongozwa na Dk Harisson Mwakyembe ambayo ilibaini namna ambavyo baadhi ya viongozi, akiwamo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu.
Wafanyakazi wa Tanesco walisema jana kwamba viongozi hao wameshiriki katika kulidhoofisha shirika hilo, hivyo wanastahili kushitakiwa na siyo kujiuzulu tu.
Source: Habari Leo, 29/02/2008
This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.
Saturday, March 01, 2008
Richmond yawatia nyongo Tanesco
Posted by
Godfrey
at
01:02
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment