WAFANYAKAZI wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), wametishia kuwaburuza mahakamani watu walioingia mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura kati ya shirika hilo na Kampuni ya Richmond.
Aidha, wafanyakazi hao wametaka kusimamishwa malipo kwa Kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba huo.
Wafanyakazi hao walitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa kujadili masuala mbalimbali ya shirika hilo na kueleza kushangazwa na kitendo cha kuendelea kuilipa kampuni ambayo msingi wake unatokana na mkataba uliohusisha kampuni hewa.
Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano ya wafanyakazi hao, Abdul Mkama, alisema hakuna sababu kwa Tanesco kuendelea kuilipa shilingi milioni 152 kwa siku, kampuni ambayo imedhihirika kuwa ilishinda zabuni kifisadi.
Sambamba na hayo, alisema ni vema watu waliojiuzulu wakarudisha fedha hizo kama inavyofanyika kwa watu waliochukua fedha katika akaunti ya malipo ya nje (EPA), na baada ya kufanya hivyo, wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Sisi wafanyakazi wa Tanesco, tunataka malipo yanayofanyika kwa Richmond yasimamishwe kuanzia leo (jana), na tunafanya taratibu, ili wahusika watulipe fidia, wasipofanya hivyo tutawaburuza kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mkama.
Naye, Balton Mwaifugile, alisema viongozi waliojiuzulu ni sehemu ndogo ya mafisadi, hivyo ni vema waliobakia nao wakaanikwa hadharani, ili kukomesha tabia ya kufuja mali za umma kwa maslahi binafsi.
Alisema wanachohitaji wao ni kulipwa fidia kwa hasara iliyopatikana, kwani fedha hizo ni nyingi na zingewasaidia kuboresha maisha yao na mitambo ya shirika hilo.
“Tunawalipa hawa jamaa wa Richmond milioni 152 kwa siku, Songas milioni 200 kwa siku na IPTL sh bilioni tatu kwa mwezi. Fedha hizi ni nyingi, na kuanzia leo tunataka tuanze kuwashughulikia kwa kutowapa fedha,” alisema Mwaifugile.
Alisema maisha ya wafanyakazi yamekuwa magumu na kupata majanga mbalimbali yaliyowasababishia ulemavu, huku wakilipwa fidia kidogo kwa madai shirika halina uwezo wa kuwalipa kutokana na fedha nyingi kuchukuliwa na mafisadi.
“Kabla ya ‘kuwanyonga’ mafisadi wetu, kwanza watulipe fidia kutokana na matatizo waliyotusababishia, ili na sisi tuishi kwa raha na kuendesha magari kama wanavyofanya wao na familia zao,” alisema Mwaifugile.
Kwa upande wake, John Mwandika, alisema hivi sasa kuna bomu kubwa linakuja nchini, kwani mradi wa kuzalisha makaa ya mawe ya Kiwira nao unatarajia kuanza kulipwa sh milioni 300 kwa siku utakapoanza uzalishaji.
Alisema mradi huo wa Kiwira utakuwa unatumia sh bilioni tisa kwa mwezi, gharama ambazo zinadaiwa zitabebwa na Tanesco, ambayo inaonekana mnyonge na sehemu ya kuchuma.
“Tanesco imefanywa mti wa mzambarau, kila mtu anakuja na kapu lake na kutingisha matunda, na kapu linapojaa huondoka na matunda,” alisema Mwandika.
Aidha, Thomas Njama, alisema wabunge wa Tanzania ni waoga, kwani suala la ubadhirifu katika Tanesco lilianza kwa menejimenti ya Net Group Solution ambayo kwa kiasi kikubwa ilivuruga muundo mzima wa shirika hilo.
Alisema uongozi huo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, wamefanikiwa kuuza majengo mbalimbali ya Tanesco, ikiwepo kutoa Chuo cha Morogoro na kuuza kiwanda cha kukaanga nguzo kilichopo Mbeya.
Aidha, alisema ni vema kuanzia sasa Katiba ya Tanzania ikabadilishwa, ili kuweza kuwakamata marais ambao watakuwa wamefuja mali za umma kwa maslahi binafsi.
Alisema Mkapa alikuwa kinara wa kushinikiza mabadiliko katika shirika hilo kwa maslahi ya watu wachache, bila kuangalia athari kwa taifa.
“Hii katiba inayotoa kinga ya kutowashtaki marais pindi wanapondoka madarakani imepitwa na wakati, inafaa tuibadilishe, ili tuweze kumkaanga Mkapa,” alisema Njama.
Source: Tanzania Daima, 01/03/2008
This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.
Saturday, March 01, 2008
Richmond yaibua makubwa TANESCO
Posted by
Godfrey
at
16:02
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment