This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.

Wednesday, January 16, 2008

Ewura kudhibiti bei ya umeme sekta binafsi

WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi amesema kwamba Mamalaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) itaendelea kuratibu bei za umeme wakati sekta binafsi itakapoanza kuzalisha nishati hiyo kuepusha wazalishaji kujipangia bei.

Karamagi alisema jana kuwa Ewura ndicho chombo cha serikali ambacho kitaendelea na jukumu hilo la uratibu baada ya sheria ya kuliondolea ukiritimba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) itakapoanza kutumika.

Muswada huo ambao jana ulikuwa unajadiliwa na wadau mbalimbali utawasilishwa katika kikao kijacho cha Bunge. Muswada huo una lengo la kuiwezesha sekta ya umeme iwe bora na inayopatikana kwa bei nafuu.

Waziri alisema uwekezaji wa umeme ni gharama kubwa hivyo anaamini kuwa wawekezaji kwenye sekta hiyo watakuwa wachache hali itakayolazimu Ewura kuendelea kuratibu bei hizo.

“Labda kwa hapo baadaye wanaweza kuwa wengi hivyo serikali inaweza kuruhusu kila mtu kujipangia bei yake, lakini kwa kuanzia naamini ewura wataendelea na jukumu hilo,” alisema wakati anazungumza kwenye kikao cha kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara.

Awali wadau walitahadharisha kuwa wawekezaji hao wanaweza kujipangia bei kama ilivyo katika sekta za simu na benki hivyo kusababisha kusiwepo na unafuu wa nishati hiyo.

Wadau hao pia waliomba serikali kutunga sheria zitakazowabana wawekezaji hao wasiweze kuanzisha mradi wa umeme na baadaye wakafunga mradi huo hali ambayo inaweza kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Waliipongeza hatua ya serikali kuandaa muswada huo ambao utafuta sheria ya umeme ya mwaka 1931 ambao ulikuwa unaipa haki Tanesco pekee kuwa wazalishaji, wasambazaji wa umeme.

Source: HabariLeo; Wednesday,January 16, 2008 @00:05

No comments: