Nishati ya miti yachangia kutunza mazingira
Nishati ya miti yachangia kutunza mazingira
2007-09-06 10:37:44
Na Moris Lyimo
Nipashe
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kutumia nishati itokanayo na miti hivyo kufanya mabadiliko ya kasi ya tabia nchi.
Ushirikiano wa serikali za Tanzania na Ujerumani (GTZ) umekuja na teknolojia rafiki wa mazingira inayolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kutumia majiko yatambulikanayo kama Roketi. Mwandishi Moris Lyimo anaelezea zaidi
Mbinu mbalimbali zimekuwa zikifanyika kupata suluhisho la kudumu la uharibifu na uchafunzi wa mazingira ambavyo vimekuwa na athari mbaya katika maisha.
Uharibifu na uchafunzi wa mazingira unaelezewa kuwa, ni kikwazo cha maendeleo ya nchi zinazoendelea, hasa katika uzalishaji wa mazao, kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi kuwa jangwa na ongezeko la joto.
Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zinazotambulikana kama AFRIKUSA zikiwemo nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinaongoza kwa kutumia nishati itokanayo na miti.
Tafiti zinabainisha kuwa sababu kubwa ni umasikini wa kipato unaokabili zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wake ikiwemo
Tanzania, kutokana na sehemu kubwa ya jamii katika nchi hizo kuishi maisha ya umasikini uliokithiri kwa mfano, kula chakula chenye thamani ya nusu hadi dola moja kwa siku.
Kutokana na hali hiyo, jamii hizo hulazimika kufanya shughuli zenye madhara makubwa kwa taifa, mfano ukataji wa mkaa, uuzaji wa magogo na kuni, lengo ikiwa ni jitihada zao za mwisho katika kujitafutia rikizi.
Matokeo yake mandhari na tabia ya nchi hubadilika na zaidi ongezeko la joto kutokana na ukame, shughuli za uzalishaji mali kusuasua (mfano kilimo) hivyo kuwa na ongezeko la kizazi kinachoishi katika umasikini mkubwa.
Katika kukabiliana na hali hiyo, wataalamu hapa nchini walikwenda nchini Ujerumani kupitia ushirikiano wa GTZ ili kujifunza mbinu endelevu baada ya kuwepo kwa mafanikio makubwa ya teknolojia ya majiko ya Roketi yaliyoanza kutengenezwa nchini humo mwaka 1997 chini ya programu inayohifadhi nishati itokanayo na tungamotaka inayotambulika kitaalamu kama Programme for Biomass Energy Conservation (ProBEC).
Mratibu wa Taifa (ProBEC-Tanzania) Bw.Arfaksad Ndilanha ambaye pia ni miongoni mwa wataalamu wa nchini waliokwenda kujifunza nchini Ujerumani anasema GTZ inaendesha mradi huo katika nchi 8 wanachama wa SADC kati ya wanachama 14 wa jumuiya hiyo.
Chanzo cha mradi huo anasema ni tatizo au kero za nchi za SADC kutokana na wananchi wake kuwa vinara wa ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa ya kuni.
Mbaya zaidi, anasema matumizi hayo si ya kisayansi kutokana na nishati hiyo kupotea ovyo sababu ya mfumo wa mafiga matatu unaotumika zaidi vijijini au matumizi ya majiko ya chuma ya mkaa, ambayo si sahihi kutumika kwenye nishati itokanayo na miti.
``Tumeona matumizi hayo husababisha njaa isiyokoma au kukoma kwa muda katika nchi nyingi za SADC, na nchi nyingine za AFRKUSA...matokeo yake ni umasikini kutokana na kuibuka kwa vikwazo vya shughuli za kilimo, ambapo zaidi ya watu asilimia 90 hutegemea shughuli hiyo na nyingine zinazoambatana,\"anasema.
Vyanzo vingine ni kilimo cha kuhama hama, mmomonyoko wa udongo, uchomaji moto misitu hivyo kusababisha tija kupungua na hatimaye umasikini.
Anasema kabla ya ujio wa teknolojia hiyo, wakuu wa nchi za SADC wamekuwa wakikutana kwa nia ya kupata suluhisho bila mafanikio ambapo kufikia mwaka 2004, teknolojia ya Kijerumani ya majiko ya Roketi iliingia Tanzania na kuanza kutekelezwa mwaka 2005, ambapo nchi za Uholanzi na Ujerumani zilijitokeza kusaidia ufanikishaji wake, ikiwemo kusambaza elimu maeneo yenye matatizo katika nchi hizo kwa awamu.
Awamu ya kwanza ilikuwa 2004/2006 ambapo ilikuwa ni kusambaza teknolojia yenyewe kwa vitendo ya namna ya utengenezaji wa majiko, kutangaza teknolojia yenyewe, na namna ya kutumia majumbani na katika taasisi binafsi na za serikali wakiwemo wafanyabiashara wadogo kama vile mama na baba lishe.
Aidha awamu hiyo ambayo ilikoma Desemba mwaka jana, ilikuwa na shughuli za kuelezea teknolojia ya ProBEC katika nchi zote za SADC baada ya kuonyesha manufaa katika nchi chache ikiwemo Tanzania.
Anasema ingawa walengwa ni waharibifu wakubwa wa mazingira katika nchi hizo, pia lengo ni kuwasaidia watu wenye kipato kidogo mijini na vijijini ambapo pindi watumiapo majiko hayo.
\"Pamoja na kusaidia katika uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa mazingira, ni teknolojia nzuri ya kiuchumi kwani mlengwa hutumia fedha kidogo kwa matumizi ya mapishi majumbani, na hata kwenye taasisi...itasaidia sana watu wenye kipato cha chini kwa sababu ya matumizi ya kuni kidogo,\"anasema Bw.Ndilanha.
Nchi zilizowahi kufikiwa na teknolojia hiyo upande wa kusini ni pamoja na Lesotho, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, na Zimbabwe wakati upande wa kaskazini unazijumuisha nchi za Tanzania, Malawi na Zambia.
Kwa hapa nchini majiko hayo yametengenezwa na kusambazwa katika makampuni ya chai na tumbaku iliyopo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, taasisi binafsi na pia kwa wakulima.
Anasema pamoja na makampuni hayo, Jeshi la Magereza pia ni miongoni mwa maeneo yaliyolengwa na teknolojia hiyo, kutokana na ukweli kuwa lenyewe hutumia zaidi nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia wafungwa.
Hadi sasa, teknolojia hiyo imeonekana kukubalika mapema, hasa baada ya wananchi kuelimishwa namna ya utengenezaji na matumizi yake katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Dar Es Salaam, Mwanza na Zanzibar.
Baadhi ya taasisi zilizopatiwa mafunzo ya namna ya kutengeneza na kutumia majiko hayo ni Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruaha, Kampuni ya Chai ya Kibena ya Njombe mkoani Iringa, wakulima wa tumbaku Iringa, Kampuni ya Chai Mufindi na pia asasi ya Emmanuel International ya Njombe mkoani Iringa.
Nyingine ni kampuni ya chai ya Uniliver na ya tumbaku ya Tukuyu mkoani Mbeya, ingawa anasema mpango ni kufika kila kona na hapa nchi, walengwa wakubwa ni maeneo ya vijijini ambapo hutumia teknolojia dhaifu (mafiga matatu) wakati wa kupika isiyoendana na wakati kwa maana ya kuhifadhi upotevu wa nishati yenyewe.
Mpango wa kuendeleza teknolojia hiyo kwa maeneo mengi, anasema imeingizwa katika awamu ya pili ya progarmu hiyo ( ProBEC phase II) iliyoanza Januari mwaka huu na lengo ni kufikia asilimia 95 ya matumizi yake.
Katika awamu hii ya pili, mpango ni kusambaza majiko ya roketi katika ukanda unaotambulika kama `Uhuru Kordo\' yenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na Pwani.
Mpango wa baadaye wa GTZ, ni tekonojia hiyo kuwafikia zaidi ya watu wapatao 800,000 ifikapo Mei 2008 inapokoma awamu ya pili ya programu hiyo.
Sanjari na faida za kiuchumi, majiko hayo husaidia usalama wa afya yatumikapo kutokana na kumudu kuhifadhi moshi jambo ambalo huepusha kuathiri mapafu, macho na kuendelea kushusha kinga ya mwili kwa wagonjwa wa ukimwi.
This blog contains information about what is happening in energy access development in Tanzania. You are welcome to give your thoughts and ideas on the issues published. Thank you.
Tuesday, September 25, 2007
Nishati ya miti yachangia kutunza mazingira
Posted by
Godfrey
at
07:34
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment